Kwako Nelson,
Ni mengi yamesemwa juu yako ndani ya majuma machache yaliyopita-kama si miezi (juu ya uwepo wako kiafya na pia sikuzo za kuwepo dunia hii ya Maulana),
Wale wasio na haya na hata kukosa hekima (pasi kuogopa asili yetu iliyotukuka ya Uafrika) wanaoweka maslahi ya kifedha mbele kupitia jinalo, lililotukuka,
Kwako Tata,
Kwa hakika Mungu (Muumba wa vyote) ndie pekee atuhuishae na aamuapo basi pasi shaka kurudi kwake,
Uongezewe rehema Nelson, Maisha yaliyo marefu pasi kutabirika Madiba
Wewe ni Jabali Dalibhunga, wewe ni mfano usiomithilika kwa mamilioni Khulu
Kwa hakika Afrika haingeweza kujivuna na kusimama kifua mbele pasipo watu mahiri na wenye Hekima kama wewe Rolihlahla
Acha waongee Nelson, acha wapaze sauti Jabali la Afrika (mawio mpaka machweo, waamkapo mpaka walalapo)
Madiba, nifikiriapo mwangu fikirani kwa watu mithili ya kwako, wale watangulizao Amani, pasi choyo ndani ya yao Mioyo, kujali wasio na uwezo tena walio katika wingi makwazo, Upendo, Mioyo iliyojaa utoaji na uhudumiaji pasipo chuki wala visasi, walio na wingi wa Usamehevu, Tata umetujaza heshima yenye wingi wa hekima, usamehevu, uvumilivu, utu uliojaa wingi wa hekima na uthaminifu,
Niangaliapo watu kama wewe Dalibhunga, najisikia kucheza ngoma zetu sadifu zilizojaa utajiri wa tungo tena zisizokifu-bara letu jadidu la Afrika (furaha yakinifu, amani isiyosadikika bali kuaminika), wewe ni kioo kamwe kisichofisha Madiba,
Kwa hakika ni kwa wachache kama wewe ambao maneno kamwe hayawezi kutosha, tuyafifkiriayo kinagaubaga kuyafikisha, utukufu wako kutonasibika,
Wewe ni shujaa Madiba, Wewe ni JABALI daima fahari kutupatia,
Alama iliyo pevu ya UAFRIKA, Tata, Rolihlahla, Dalibhunga
Uongezewa rehema Madiba, Uishi maisha marefu (zaidi na zaidi) Rolihlahla,
Umkotho WeSizwe,
Matukio OleAfrika Aranyande Chuma
Monday, August 31, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment